Alhamisi , 16th Jul , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amesema kuwa vijana wengi ambao wamezaliwa miaka ya 1982, hawaridhiki na nafasi walizonazo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo hii leo Julai 16, 2020, Ikulu ya Chamwino, Dodoma, mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwaapisha viongozi aliowateua, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya mbalimbali hapa nchini.

"Hii kazi umeipata kwa sababu Mungu alitaka, mkamtangulize Mungu katika kazi zenu lakini pia mkawatumikie wananchi maskini katika maeneo yenu, nipende kusisitiza kwamba katika kazi hizi, kuridhika ni jambo muhimu sana, unajua vijana saa nyingine hawaridhiki harakaharaka haswa waliozaliwa miaka ya 1982" amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amesisitiza kuwa katika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba, wananchi wasishawishiwe na wagombea ya kwamba amewatuma yeye, kwa kuwa hakuna mgombea aliyetumwa na Makamu wa Rais wala Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Mzee Philip Mangula.