Alhamisi , 9th Oct , 2014

Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini Tanzania wameitaka serikali kuhakikisha inatumia utajiri wa rasilimali mbalimbali za nchi kuwaunganisha watanzania na sio kutumia rasilimali hizo kwa ajili ya kuwagawa na kuvunja amani ya nchi.

Askofu wa Jimbo Katoliki Jimbo la Mwanza Askofu Yuda Thadeus Ruwaichi.

Kauli hiyo imo ndani ya tamko la pamoja walilolitoa viongozi hao baada ya mkutano wao wa siku nne uliowakutanisha viongozi wa dini ya kikristi na Kiislamu ambao walikuwa wakikutana chini ya mwamvuli wa Mpango wa Mahusiano Bora baina ya Waislamu na Wakristo Barani Afrika au kwa kifupi PROCMURA.

Akitoa tamko hilo kwa niaba ya viongozi wenzake, Askofu wa Jimbo Katoliki Jimbo la Mwanza Askofu Yuda Thadeus Ruwaichi amesema mbali ya rasilimali, serikali pia iache kutumia nguvu kupita kiasi inaposhughulikia matukio ya uvunjifu wa amani sambamba na kuimarisha ulinzi kwenye mikusanyiko ya watu pamoja na nyumba za ibada.

Kwa mujibu wa askofu Ruwaichi, wao kama viongozi wa dini wataendelea na jukumu la kuwaunganisha waumini wao na kufundisha mafundisho mema yatakayowajenga na kuwa watu wema katika jamii.

Aidhaa amesema watahakikisha waumini wa dini zote nchini wanaendelea kuheshimiana pasipo kujali tofauti zao za kiimani huku wakidumisha upendo na amani ya nchi.