Jumatatu , 19th Feb , 2018

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha kila shule ya sekondari inayojengwa inajengwa ikiwa na maabara.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi Lamadi wilaya ya Busega mkoani Simiyu ikiwa siku yake ya kwanza ya ziara ya siku tano mkoani humo.

Mh. Suluhu ambaye alianza ziara yake kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji uliopo Kiloleli ambapo mradi huo ukikamilika utasaidia kupatikana kwa maji safi na salama kwa vijiji vitatu na utagharimu shilingi za Kitanzania Bilioni 1.6 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 80%.

Aidha amewapongeza Makamu wananchi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano katika uwekezaji na uendelezaji wa viwa nda ambapo mpaka sasa kuna viwanda 14 vya usindikaji wa pamba na viwanda vidogo vidogo vya usindikaji mazao 1,035.

“Nawapongeza kwa mkakati wa kuzalisha bidhaa za afya zinazotokana na pamba na maji ya drip”

Makamu wa Rais aliwaambia wananchi hao kuwa hadi mwisho wa mwezi huu chupa milioni 2 za dawa za kuuwa wadudu wanaoshambulia pamba zitakuwa zimesambazwa.