Ijumaa , 11th Jul , 2014

Serikali imewataka viongozi na watendaji wa jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa wanatoa kipaumbele na kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na vitendo vyote vinavyochangia maambukizi mapya ya VVU katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Mkuu wa mko wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadick

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadick jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya siku nne ya viongozi na watendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam.

Bw. Sadick amesema viongozi na watendaji wa jiji ndio wenye dhamana na jukumu la kusimamia na kuongoza mipango yote ya mapambano ya maambukizi mapya ya VVU wakishirikiana na wananchi na kufafanua kuwa janga la Ukimwi lisipodhibitiwa katika ngazi zote litaendelea kupoteza nguvu kazi na kuiongezea serikali mzigo wa kuwahudumia wagonjwa wapya.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, moja ya maeneo ambayo viongozi hao wanaweza kushiriki katika kupunguza maambukizi mapya ni kupitia elimu kwa umma juu ya madhara na hatari ya ugonjwa wa UKIMWI, hususani katika maeneo yao ya kiutawala.

Mkuu wa mkoa Sadick amesema wananchi wapaswa kufahamishwa na kupewa elimu kuhusu umuhimu wa wao kujikinga kwa kuacha ngono zembe pamoja na uaminifu baina ya wapenzi na wanandoa.