Jumatatu , 12th Sep , 2016

Vijana nchini wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza na kuto kutegemea ajira za kuajiriwa kwenye maofisi ya umma au binafsi.

Kauli hiyo imetolewa na mdau wa maendeleo nchini bwana Eric Shigogo kwenye tamasha maalum lililopewa jina la Campus Night lililoandaliwa maalum kwaajili ya vijana wote nchini lengo likiwa ni kuwahamasisha na kuwafundisha namna yakutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza nchini hasa zile za kimazingira na kuachana na mawazo ya kimasikini ambayo hayataweza kusaidia taifa kufikia nchi ya uchumi wa kati.

Amesema bado kuna vijana wengi wapo kwenye dimbwi la umaskini wakati taifa la Tanzania limebarikiwa maliasili za kuongeza utajiri wa wananchi wake, na kuongeza kuwa taifa lina fursa nyingi sana na kuwataka vijana kujiingiza katika kufanya shughuli zao mbalimbali za kuongeza vipato vyao na kila mmoja awajibike katika kutumia vipaji vyake na kutimiza ndoto zake.

Kwa upande wake mtaalam wa Saikolojia na familia kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam Dkt. Chris Mauki amesema ni vijana zaidi ya asilimia 60 ya watu Tanzania watapata mbinu za kutumia fursa mbalimbali ambazo zitawawezesha kupata njia sahihi za kutatua matatizo yao hasa yale ya ajira.

Amesema vijana wengi wanakosea kwenye kuwaza fikra zilizopinda na kuamini hawawezi kufanya mageuzi ya maisha yao, hivyo ni lazima wakubali mabadiliko kuanzia kwenye fikra zao binafsi ili waweze kujenga na kufikia malengo yao waliyojiwekea.

Kwa upande wake muandaaji wa tamasha hilo Bwana Prosper Mwakitalima amesema tamasha hilo limelenga kuwafikia vijana wengi nchini kwa kutumia sanaa mbalimbali kwakuwa vijana wengi ndiyo taifa ambalo linategemewa kwa miaka ya baadaye, hivyo ni lazima kuhakikisha kundi hilo linakuwa katika maadili mema na kuwabadilisha kuanzia ndani ya nafsi zao mpaka nje.