Jumatano , 27th Apr , 2016

Mamia ya vijana katika Manispaa ya Musoma wamekosa ajira kutokana na kufungwa kwa viwanda vitatu vikubwa vikiwemo vya kuchakata samaki kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa mitaji na malighafi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Magesa Mulungo

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Magesa Mulungo, amefanya ziara katika viwanda hivyo vilivyofungwa kujionea hali ilivyo na kuweka mikakati ya kuona namna bora ya kusaidia ili viwanda hivyo kuanza kufanya kazi ili kuongeza pato la mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla.

Katika ziara yake hiyo Mkuu huyo wa mkoa amekitaka kiwanda kimoja kati ya vilivyofungwa kuanza kufanya kazi mara moja kutokana na kutoridhishwa na maelezo ya sababu zilizofanya kufungwa kwa kiwanda hicho wakati samaki kwa sasa wapo, licha ya kuwapo changamoto za uvuvi haramu.

Aidha, Bw. Magesa amesema kuwa ataziita mamlaka husika kukaa pamoja ili kuangalia mustakabali wa viwanda hivyo kwa mtazamo wa maendeleo ya jamii na sio kwa muwekezaji pekee ili kuokoa maisha ya wakazi wa Mara na taifa kwa ujumla.

Aidha, amesema kuwa atakaa na wamiliki wa viwanda vyote mkoani humo kuona changamoto gani zinawakabili ili serikali ya mkoa kwa ushirikiano na serikali kuu iweze kuweka mipango ya kusaidia viwanda hivyo vifanyekazi kwa kiwango cha hali ya juu.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulungo akizungumza namna wa kuvisadia viwanda mkoani humo