Ijumaa , 14th Jul , 2023

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu imefungua rasmi ushirikiano na vyuo vya ufundi vya nchini China ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa kitanzania kusoma na kuja kufanya kazi katika miradi ambayo inaendeshwa na makampuni kutoka China hapa nchini.

Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda

Akifungua ushirikiano huo Waziri wa Elimu Prof Adolf Mkenda amesema Tanzania na China zinaushirikiano wa muda mrefu kwenye sekta mbalimbali ikiwemo uchumi,siasa na sasa uwekezaji huu umeelekezwa kwenye sekta ya elimu katika vyuo vya ufundi ili kuwasaidia watanzania vijana kupata wataalam ambao watafanya kazi miradi mbalimbali.

"Tuko na vyuo vingi vya ufundi sasa ni kweli wenzetu wachina wameendelea sana katika teknolojia hivyo kupitia utaratibu wa vijana kwenda huko kusoma watakuwa na vigezo vya kuajirika kirahisi zaidi na tayari vijana kadhaa wameanza kwenda kutoka vyuo vya ufundi kadhaa," amesema Prof Mkenda

Hata hivyo kwa upande wao Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET)amesema hii leo tayari vyuo 30 mbalimbali vya ufundi kutoka China vimehudhuria katika semina ya kujadili na kuingia mikataba ya awali na vyuo mbali mbalimbali vya ufundi kutoka hapa Tanzania.

"Kwa wanafunzi ambao wanasoma degree watapata fursa ya kusoma miaka miwili china na mingine miwili Tanzania ambapo ndani ya shahada yake ndani yake  atakuwa ngazi ya diploma ya ufundi kutoka China ambayo ataweza kuajirika hapa kwenye makampuni yao,"  amesema Adolf Rutayugwa-Katibu Mtendaji NACTVET.