Jumapili , 10th Sep , 2023

Idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi nchini Morocco imeongezeka na kufikia zaidi ya 2,000, huku idadi sawa na hiyo ikiwa ni majeruhi.

Morocco

Wizara ya Mambo ya Ndani imesema zaidi ya watu 1,400 wana majeraha mabaya, na idadi kubwa ya majeruhi ni katika majimbo ya kusini mwa Marrakesh.

Mfalme Mohammed VI alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa na kuagiza makazi, chakula na msaada mwingine kwa manusura. Watu wengi wametumia  usiku wa pili nje kwenye maeneo ya wazi.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.8 lilipiga mji wa Marrakesh na miji mingi siku ya Ijumaa usiku ambapo katika maeneo ya milimani, vijiji vyote vinaripotiwa kuwa vimeharibiwa.