"Uzalendo siyo kutukuza asubuhi hadi jioni"- MCT

Jumatatu , 3rd Mei , 2021

Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, amesema kuwa uzalendo kwa nchi siyo kutukuza kuanzia asubuhi hadi jioni bali uzalendo ni kuipenda nchi yako na kuhakikisha mtu anaisema serikali mahali ambapo ataona kuna jambo ambalo halitoleta afya kwa Taifa.

Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga

Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 3, 2021, kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, wakati Dunia ikiadhimisha siku ya Uhuru wa Vyomba vya Habari, huku akiwasihi waandishi wa habari kutokubali kuyumbishwa kwa maslahi ya mtu.

"Uzalendo ni kuipenda nchi yako, kuiheshimu na kuwa na uchungu na nchi yako, uzalendo siyo kuipenda serikali, uzalendo siyo kumpenda Rais, uzalendo ni zaidi ya hapo, uzalendo ni uwezo wa kusema serikali hapa imekosea hili jambo si jema kwa nchi yako na kulitamka, uzalendo siyo kutukuza asubuhi hadi jioni,  uzalendo ni kujadili kwa nia njema maendeleo ya nchi", amesema Mukajanga.

Akizungumzia kuhusu suala la mwelekeo wa vyombo vya habari kuwa huru, Mukajanga amesema, "Mwelekeo wa uhuru wa vyombo vya habari upo kwa sababu matamko ya mkuu wa nchi yanabeba uzito mkubwa na matamko ya Rais Samia yanaelekea huko na jukumu letu kama wanahabari tumepewa mazingira ambayo tunaweza tukasema kwa uhuru zaidi, tunaweza tukadai haki zetu pia tunaweza tukaingia katika mjadala wenye tija".