Jumamosi , 25th Mar , 2023

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim M. Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ghala la nafaka katika Kijiji cha Ikindilo, Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu

Ameitaka Wizara ya Kilimo kuhakikisha inasimamia kikamilifu uendeshaji wa ghala hilo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 1500 za nafaka ili lilete manufaa kwa wakulima wa Wilaya ya Itilima

Katika hatua nyingine Mh Waziri Mkuu Majaliwa amepokea  maombi kutoka kwa wabunge wa Mkoa wa Simiyu wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Itilima Mh Njalu Silanga juu ya usimamizi wa ghala hilo la nafaka kuwa chini ya NFRA ili kuongeza ufanisi.

Akiulezea manufaa ya mradi huo Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde amesema mradi huo wa ujenzi wa ghala unalenga kwenye udhibiti wa sumukuvu na kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno kwa kuhusisha ujenzi wa ghala lenye uwezo wa kuhifadhi tani 1500 za nafaka,maabara,sehemu ya kukaushia nafaka na vifaa vya kisasa vya maabara.

“Kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na usaidizi wako Mheshimiwa Waziri mkuu kwa kazi kubwa inayofanyika katika Sekta ya Kilimo….Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maelekezo ambayo umenipatia hapa naomba niutamkie umma wa wananchi wa Itilima ya kwamba Ghala hili ambalo lipo chini ya Halmashauri tutawakabidhi pia Wakala wa Uhifadhi wa Chakula Tanzania (NFRA) kwa ajili ya uendeshaji wake ili kuongeza ufanisi”Alisema Mavunde