Baadhi ya vijana wa CCM katika wilaya ya Bunda mkoani Mara wamesema kuporomoka kwa ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa kumesababishwa na udhaifu wa viongozi wa juu wa serikali wa kutolishughulikia kwa haraka sakata la Escrow.
Wakitoa maoni yao kwenye kikao cha baraza la Umoja wa Vijana (UVCCM) la wilayani humo lililofanyika jana,
vijana hao walisema kutokana na hali hiyo wananchi walikosa imani kwa serikali ya CCM na hivyo kuamua kukinyima kura katika uchaguzi huo.
Akisisitiza maoni hayo, mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya hiyo, Flavian Nyamageko alisema pamoja na ushindi kilioupata chama hicho katika uchaguzi huo, kilipata msukosuko mkubwa kutokana na sakata la Escrow na ujenzi wa maabara.
Kwa upande wake mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa Robert Maboto aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao hicho alielezea usaliti wa baadhi ya wanachama na tabia ya kulazimisha kugombea hata kama hupendwi kama sababu pia zilizoporomosha ushindi wa chama hicho.
Awali katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo Adonias Magoma alisema lengo la kikao hicho ni kujitathimini kama chama kilifanya vizuri katika uchaguzi huo huku akisema ushindi kilioupata siyo saizi yake.
Nao baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walitoa maoni yao kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana pamoja na mustakabali wa siasa ndani ya chama hicho.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Desemba 14 mwaka jana, CCM wilayani Bunda ilipata jumla ya vijiji 77 sawa na asilimia 72 ya vijiji vyote 107 vya wilayani humo huku kikipata vitongoji 422 kati ya 566 vya wilaya hiyo sawa na asilimia 75 huku UKAWA ukiambulia vijiji 30 na vitongoji 144.