Baadhi ya Wakimbizi kutoka nchini Burundi wakiwasilini nchini Tanzania
Katika taarifa iliyotolewa, UNHCR imesema kuwa wakimbizi saba wameshafariki dunia tangu Ijumaa, wawili wakiwa wamebainishwa kuwa na dalili za kipindupindu.
Aidha, Warundi 77 kwenye kambi ya Nyarugusu, magharibi mwa mkoa wa Kigoma, na wengine 300 kwenye kijiji cha Kagunga nchini Burundi na Kigoma nchini Tanzania wanatibiwa maradhi ya ugonjwa wa kuharisha.
Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania, Joyce Mends-Cole amesema kipaumbele cha shirika hilo ni kushirikiana na wizara ya afya ili kufungua haraka kituo cha kutibu kipindupindu kwenye kijiji cha Kagunga, akieleza kwamba kuna kituo kimoja kidogo tu cha afya kwenye kijiji hicho.
Halikadhalika UNHCR inachukua hatua za kuimarisha usafi na mifumo ya kusafisha maji machafu, pamoja na kuhamisha wakimbizi kutoka Kagunga hadi kigoma na kambi ya Nyarugusu
Kwa mujibu wa mamlaka za serikali ya Tanzania, idadi ya wakimbizi kutoka Burundi imefikia 70,000 nchini Tanzania, 50,000 wakiwa wanaishi kwenye mazingira magumu kwenye kijiji cha Kagunga.