
Akiongea na www.eatv.tv Prof. Ngowi amesema kwa miaka karibuni serikali ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki zimekuwa zikiweaka nguvu katika ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na viwanja vya ndege na kuongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 inategemewa kutengwa kiasi cha jumla ya shilingi trilioni 32.
“Nadhani itakuwa kama Bajeti ya miaka miwili au mitatu iliyopita kimsingi inaweza kufika trilioni 32 na tutegemee kiasi kikubwa kitaenda katika matumizi ya kawaida kuliko matumizi ya maendeleo labda kwa asilimia 70 kwa 30, lakini tutegemee kiasi kikubwa sana kitaenda katika miundombinu kwasababu ndiyo inaonekana ni mkazo kwa Afrika Mashariki yote” amesema Profesa Ngowi.
Katika upande wa mapato Prof. Ngowi amedai kuwa hakutakuwa na mabadiriko makubwa sana katika ukusanyaji wa kodi kwasababu hali ya uchumi wa nchi hairuhusu kuwa na ongezeko jipya la kodi.
“Hali ya uchumi wa sasa sitegemei kuwe na kodi nyingi zaidi na kodi mpya kubwa, naamini hali ya kodi itabakia kama ilivyo na ingepaswa baadhi ya kodi zipunguzwe kwa maana ya aina ya kodi na wingi wa viwango vya kodi” ameongeza Prof. Ngowi
Profesa huyo wa uchumi amependekeza kuwe na sera pana za kodi kuwezesha kukuza uchumi wa nchi na kurahisisha ulaji zaidi kwa wanachi na kutaka bajeti ya mwaka huu isiongeze kodi katika matumizi wa kila siku ya mwanachi wa kawaida.
Leo Juni 14, 2018 Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, atawasilisha Bungeni bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Jijini Dodoma.