TPDC imesema mradi huo wa mabomba ya gesi unatarajiwa kukabidhiwa kwa serikali ifikapo Juni mwaka huu.
Akiongea jijini Dar es Salaam leo mwenyekiti wa bodi ya TPDC Michael Mwanda amesema utekelezaji wa mradi huo utaiwezesha Tanzania kupata umeme wa uhakika na wa bei nafuu pamoja na utunzaji wa mazingira.
Aidha Mwanda ameongeza kwa kusema kwamba katika maeneo mitambo ya kusafirishia gesi itakapojengwa kutajengwa mitambo ya kusafishia maji safi na kuwa mpaka sasa wameshatekeleza mradi wa visima vyenye ujazo wa mita 150.
Amesema mradi wa miundombinu ya gesia asilia unahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia Madimba (Mtwara) pamoja na Songo Songo (Lindi)na Bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Mtwara, Lindi na Pwani hadi Dar es salaam.
Katika eneo la Madimba mitambo mitatu yenye uwezo wa kusafisha futi za ujazo milioni 70 kila mmoja kwa siku inajengwa.
Mitambo mingine miwili yenye uwezo wa kusafisha futi za ujazo milioni 70 kwa kila mtambo kwa siku inajengwa eneo la Songo Songo
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TPDC, Gharama za mradi huo ni Dola za Marekani 1,225,327,000 ambapo kati ya hizo, Benki ya Exim ya China imechangia 95% na serikali imechangia 5%.
Katika kiasi hicho, Mtambo wa kusafishia gesi ya Songo Songo utagharimu Dola za Marekani 151,735,000, wakati mtambo wa kusafishia gesi asilia Mnazi Bay ni Dola za marekani 197,877,000 na Bomba la kusafirishia gesi asilia likigharimu dola za Marekani 875,715,000.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC James Andilile, gharama hizo ni za chini na nafuu ukilinganisha na miradi mingine kama hiyo duniani.