Ijumaa , 23rd Sep , 2022

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amesema ujenzi wa barabara na madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe na matofali ya kuchoma unaokoa gharama kwa asilimia 50.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma, Mhandisi Seff alisema teknolojia hiyo inapunguza gharama kwasababu inatumia malighafi ambazo zinapatikana katika maeneo husika.

“Tumejenga madaraja ya mawe zaidi ya 73 Kigoma kwa shilingi bilioni 1.4 lakini pia ujenzi unaendelea katika Mkoa wa  Mwanza, Iringa na Singida ambapo bei ni nafuu na ukizingatia mawe yanapatikana katika maeneo mengi nchini,” alisema Mhandisi Seff.

Aliongeza kuwa mkakati wa TARURA ni kuanza kufundisha mafundi katika kujenga madaraja hayo ili nao waweze kufundisha wengine.


Kwa upande wake Mratibu wa madaraja ya mawe, Mhandisi Pharles Ngeleja alisema mipango iliyopo ni kuhakikisha wanawezesha mafunzo kwa wahandisi ili waweze kufahamu kwasababu wao ndio wasimamizi wa miradi.

"Bado kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi juu ya teknolojia hii lakini elimu inaendelea kutolewa na tunaamini itafika muda ambao wananchi wataielewa vizuri maana teknolojia hii ni ya gharama nafuu na huleta matokeo chanya kwani ukiangalia miundombinu mingi ya zamani ilitumia teknolojia hii", alisema.

Alisema madaraja yanayojengwa kwa kutumia teknolojia ya matofali na mawe ni imara na yana uwezo wa kukaa zaidi ya miaka 200.

"Ukiangalia nchi za wenzetu wana madaraja ambayo walijenga kwa kutumia chokaa lakini hadi leo yapo na yanafanya kazi hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi waipokee teknolojia hii", alisema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliipongeza TARURA kwa kutumia teknolojia hiyo ambayo itasaidia kuokoa fedha za serikali.

Mkazi wa Makulu Godwini Chisili alisema amevutiwa zaidi na ujenzi wa barabara na madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe na matofali kwasababu ni malighafi ambazo zinapatikana katika mikoa mingi nchini na kutokana na kupatikana kwa malighafi hizo kutasaidia serikali kupunguza gharama za ujenzi.

“Sasa tumepiga hatua tunachoomba ujenzi wa barabara na madaraja hayo uzingatie ubora na hatutegemei kuona daraja linajengwa ndani ya wiki tatu linakatika", alisema.

Aidha, ameishauri Serikali kuona umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa wazawa wakati wa utekelezaji wa miradi hii ili kuwezesha teknolojia kusambaa kwa urahisi na kutumika katika maeneo mengi yenye mawe.