Raabia Hawa, Mratibu wa matembezi ya kupiga vita ujangili wa tembo yaliyoanzia Hifadhi ya Taifa Arusha na yanatarajiwa kumalizikia Nairobi.
Mpango huo unaotekelezwa kupitia Programu ya Kilimanjaro Land Scape na Jumuiya ya Wanyamapori Enduimet na kuratibiwa na shirika la hifadhi ya wanyapori AWF unatajwa kupunguza mauaji ya wanyama wakubwa wakiwemo Tembo wanaopatikana kupitia ushoroba wa Kitenden uliopo ukanda wa kaskazini mwa nchi.
Mkuu wa usalama wa Jumuiya ya wanyapori Enduemet Charles Bujiku, amesema kupitia askari hao wanaofikia hamsini sasa ambao wanatoka ndani ya vijiji Tisa vya wanachama wa Jumuiya hiyo kumekuwako na mawasiliano mazuri baina yao na askari wa upande wa Kenya, na hivyo kudhibiti vitendo vyote vya ujangili.
Pamoja na kudhibiti ujangili, wakazi wanaoishi ndani ya jumuiya ya wanyamapori wamebainisha kupungua kwa migogoro baina ya wafugaji na wanyamapori, kwa kutekeleza mpango kabambe wa ujenzi wa uzio imara katika maboma ya wafugaji wenyeji wanaoishi ndani ya jumuiya.
Afisa maendeleo ya jamii wa AWF Kimai Lendukai anasema shirika lao linatekeleza miradi hiyo kama njia mojawapo ya kuwashirikisha wananchi katika uhifadhi wa mazingira na wanyamapori ili kuhakikisha wananchi nao wananufaika na rasilimali za wanyamapori zinazowazunguka.
Askari wa wanyama wanafanikisha program hizo baada ya kupatiwa mafunzo katika chuo cha wanyamapori Pasiansi Mwanza panoja na nchini Kenya, ikiwa ni utekelezaji wa sheria za uanzishwaji wa jumuiya za hifadhi za wanyapori ambazo zimepewa jukumu la kujiendesha zenyewe likiwemo suala la ulinzi.