
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limefanikiwa kudhibiti matukio mbalimbali ya kihalifu yanayojitokeza ndani ya Ziwa Victoria, vikiwemo vitendo vya uvuvi haramu na uporaji wa kutumia silaha, kufuatia doria zinazoendelea kufanywa na askari wa jeshi hilo kwa nyakati tofauti.
Akizungumza na wananchi wa Kisiwa cha Bezi kilichopo katika Manispaa ya Ilemela, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbroad Mutafungwa alisema kuwa, jeshi hilo linaendelea kufanya kazi kwa bidii masaa 24 ili kuhakikisha Ziwa Victoria linabaki kuwa salama kwa wananchi wote.
Kamanda Mutafungwa alibainisha kuwa doria hizo zimeleta matokeo chanya, ikiwemo kupungua kwa matukio ya kihalifu ndani ya ziwa hilo, jambo linaloongeza imani ya wananchi kwa vyombo vya dola na kuimarisha shughuli za kiuchumi zinazofanyika ndani na pembezoni mwa ziwa hilo.
Aidha, Kamanda Mutafungwa amesisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana hayawezi kuendelea bila ushirikiano wa karibu kutoka kwa wananchi, hivyo aliwaasa kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu mapema ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
Jeshi la Polisi limeendelea kujipanga zaidi kwa kuimarisha doria zake katika ziwa Victoria na maeneo ya mwambao wa ziwa hilo huku likiahidi kuchukua hatua kali kwa wote watakaobainika kushiriki katika vitendo vya kihalifu hasa wale wanaojihusisha na uvuvi haramu unaoharibu rasilimali za taifa.