Humphrey Polepole - Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM
Hayo yameelezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole alipokuwa akijibu maswali ya wananchi kupitia kipindi cha KIKAANGONI kinachoruka LIVE kila Jumatano saa 8 mchana kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV.
Polepole amesema chama hicho kwa sasa kinahitaji zaidi damu changa na vijana zaidi kuliko kinavyohitaji wazee, hivyo kama kuna mzee anahitaji kuendelea kubaki CCM anapaswa kuwa na akili zilizochangamka kama yeye ambaye ni kielelezo cha vijana.
"Tutaondoa wazee wote wasio na tija ndani ya CCM, tunataka vijana wengi zaidi na wazee wachache wenye akili kama za vijana, kama mimi, na siyo kwamba hatutakuwa na wazee, uongozi mzuri ni kuchanganya wazee na vijana, hata mimi nisingekuwa hivi kama nisingekuwa na urafiki na kama Warioba, Butiku, Augustino Ramadhani, prof. Kabudi, Richard Lyimo wa TLP na wengine wengi, kwahiyo nawashauri vijana wawatafute wazee kama hao" Alisema Polepole
Katika majibu ya swali lingine, Polepole alisema kuwa hivi sasa chama hicho kimeamua kufanya siasa safi huku akiviaka vyama vingine vya siasa kufuata nyayo za chama hicho.
"Tumeamua kufanya siasa safi na uongozi bora, na vyama vingine viige, tuache ila, tuache fitina, tushaambiana kwenye CCM"
Pia alisema kuwa chama hicho hakijiiti chenyewe kuwa ni chama cha wanyonge bali huo ndiyo ukweli wenyewe kuwa chama hicho ni chama cha mapinduzi, na mapinduzi maana yake ni kuwaepusha wanyonge dhidi ya wanyonyaji, kwahiyo kihistoria chama hicho ni cha wanyonge na kusema "Hatujiiti chama cha wanyonge, sisi ni chama cha mapinduzi".