
Kamanda Kova ameyasema hayo alipokuwa akiongea na East Africa Radio, na kusema kuwa wao kama jeshi la polisi wanataka watu wawe salama na kusherehekea sikukuu kwa amani, hivyo wamechukua hatua za kudhibiti uhalifu huo usitokee kabisa.
“Mara baada ya shughuli za uchaguzi tulianza maandalizi mapema ya kupambana na uhalifu, na sasa hivi wameshakamtwa watuhumiwa wapatao 353, wengine wameshafikishwa mahakamani, jamii ijue tu kwamba kuna kazi kubwa inafanyika, tunataka mpaka inavyofika krismas hali iwe shwari kabisa”, alisema Kamanda Kova.
Pia Kamanda Kova amewataka wananchi kutoa msaada kwa jeshi la polisi kwa kutoa taarifa wanapoona dalili za vitendo vya uhalifu, kwani wahalifu hao wanaishi na jamii.
“Wahalifu wengine waliobakia ni vizuri wananchi wakatusaidia, kwa sababu wahalifu wote wanakaa miongoni mwao, wanakaa katika nyumba moja, mtaa mmoja, watupe taarifa kwa yale mawasiliano yetu ya kawaida, kuliko mkinyamaza alafu uhalifu ukitokea mnasema polisi hawafanyi kazi”, alisema Kamanda Kova.
Pamoja na hayo Kamanda Kova amesema siku za hivi karibuni uhalifu wa kutumia silaha umepungua, ila kumeibuka vitendo vya utapeli ambavyo vimekithiri zaidi.
"Sasa hivi uhalifu wa kutumia silaha umepungua sana ingawa hatujaridhika, lakini kuna hawa matapeli au watu wanaopenda kujitafutia fedha kwa njia za ujanja ujanja sasa hivi ndo umeongezeka, hao nao tutaendelea kuwashughulikia", Alisema Kamanda Kova.
Kamanda Kova amewataka pia wazazi kuangalia watoto wao ili wasije wakajiunga na vikundi vya uhalifu akitolea mfano panya road, na kuwahimiza kuwapeleka shule kwani sasa elimu itatolewa bure.