Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard Kayombo
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa (TRA) Bw. Richard Kayombo, ameia embia EATV kuwa sukari hiyo iliingizwa nchini na kampuni ya Al-Naeem na ilikuwa ikisubiri vibali kutoka Bodi ya Sukari, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na kukamilisha taratibu za kodi.
"Baada ya kupitia na kufanya ukaguzi wa kila hatua tumejiridhisha kuwa tani 6,757 za sukari tulizokuwa tunazishikilia katika maghala ya forodha huko Mbagala zimeingizwa nchini kwa kufuata taratibu zote na hivyo tumeona hakuna haja ya kuendelea kushikilia shehena hiyo," alisema Bw. Kayombo.
Kwa mujibu wa Bw. Kayombo, mmiliki wa shehena hiyo ameruhusiwa kuanza kuisambaza sukari hiyo katika mzunguko wake wa kibiashara na kwamba kuwepo kwake sokoni huenda kukasaidia kupunguza bei na makali ya upatikanaji wa sukari nchini. Aliongeza kuwa "Tuna imani kuwa baada ya shehena hii kuingizwa sokoni, uhaba wa sukari utapungua na bei yake itarejea kuwa ya kawaida,".
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Al-Naeem Bw. Eddy Salim amesema baada ya ruhusa hiyo ya serikali, wamejipanga kuhakikisha sukari inasambazwa katika maduka yao yote huku wakihakikisha kuwa bei inabaki kuwa ya kawaida.