Ijumaa , 17th Jun , 2016

Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Tanzania – TPSF, leo imesaini makubaliano na kampuni ya Canada ijulikanayo kama CESO kwa ajili ya kujenga uwezo sekta binafsi juu ya namna ya kuendesha miradi ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF Godfrey Simbeye (kulia) akiwa na Mshauri Mkuu wa CESO Bw. Jose Jacome muda mfupi kabla ya kusaini makubaliano hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF Godfrey Simbeye amesema makubaliano hayo ni ya ushirikiano utakaodumu kwa kipindi cha miaka mitano ambapo CESO itakuwa ikiipatia TPSF pamoja na makampuni wanachama, uwezo wa kitaalamu wa namna ya kukuza sekta binafsi pamoja na uwezo wa kiushindani katika uwekezaji na biashara.

“Tunafurahi sana kusaini makubaliano haya kwani moja ya majukumu yetu ni kuhakikisha makampuni na wafanyabiashara ambao ni wanachama wa TPSF wanaendesha biashara zao kitaalamu na kuwa na ushindani wenye tija kwa mafanikio yao na uchumi wa nchi kwa ujumla,” amesema Simbeye.

Amefafanua kuwa TPSF kama chombo cha kukuza ustawi wa sekta binafsi kinakabiliwa na changamoto nyingi za kiuendeshaji kama ilivyo kwa makampuni.

“Mathalani makampuni mengi nchini yanakabiliwa na migogoro inayotokana na ukosefu wa muundo bora wa uongozi na hata ukosefu wa ujuzi....migogoro yote hii inachangia kushusha ari na ufanisi wa makampuni haya na ndiyo maana wadau wetu hawa wameamua kuja kutujengea uwezo wa jinsi ya kuendesha biashara zetu na hasa eneo la uwekezaji na ushindani katika biashara,” amesema Simbeye

Jacqueline Mndeme ni Afisa Ufuatiliaji na tathmini wa CESO hapa nchini ambapo amesema kupitia serikali ya CANADA watahakikisha wanayajengea uwezo makampuni ya ndani yaweze kukua, kushindana na kufikia masoko ya kimataifa.

“Tayari tuna taasisi mashirika ambayo tumeanza kufanya nayo kazi kama vile SIDO na mengine mengi na tutakuwa tunafuatilia kutathmini kuona kama uwezeshaji tunaoufanya unaleta tija kwa wanufaika na kuona na maeneo gani yanahitaji nguvu zaidi,” amesema Bi. Jacqueline.

Mshauri mkuu wa kampuni hiyo Bw. Jose Jacome ameelezea namna watakavyoyajengea uwezo makampuni wanachama wa TPSF huku Bw. Bryan Marshman akieleza jinsi uzoefu wake kwenye masuala ya kodi utakavyoyanufaisha makampuni ya Kitanzania.