Rais wa TLS Charles Rwechungura akizungumza jijini Arusha mwishoni mwa wiki amesema tangu kuanza kwa mchakato wa katiba mpya TLS iliunda kamati maalum kutafiti na kushughulikia mchakato huo kisheria na ndiyo imehusika na maadalizi yote ya kufungua shauri hilo.
Rwechungura amesema pia wataiomba mahakama ifafanue iwapo katiba halali kisheria itapatikana bila makundi yote ya kijamii ikiwepo UKAWA kutokuwepo bungeni.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi ambaye ni Mwenyekiti mwenza wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA, Mhe. James Mbatia ameshangazwa na kile alichokiita kuwa ni upindishaji wa sheria juu ya uhalali wa kusitishwa au kutositishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Akizungumza wakati akitoa maazimio ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyokutana jijini Dar es Salaam; Mhe. Mbatia ameonesha kushangazwa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kuwa hakuna mwenye uwezo wa kusitisha bunge hilo.
Katika maelezo yake, Mbatia amehoji ni wapi bunge hilo lilipata uhalali wa kisheria wa kusitisha vikao vyake na kupisha vikao vya bunge la bajeti, huku ishara zikionesha kuwa bado bunge hilo litahitaji muda zaidi ya ule uliomo kwenye sheria wa kuendelea na mchakato wa Katiba mpya.