Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Sophia Mjema.
Miradi hiyo kwa mujibu wa makubaliano ya mkopo huo ni ile ya ujenzi wa masoko ya kisasa, malipo ya fidia ya ardhi itakayotumika kwa ajili ya miradi hiyo pamoja na ujenzi wa barabara za lami katika mitaa yote mikubwa ya manispaa hiyo.
Akizungumza wakati wa kusaini utolewaji wa pesa hizo; Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Sophia Mjema, amesema lengo la fedha hizo ni kuboresha mandhari na kukuza vyanzo vya mapato vya manispaa hiyo ili ifanane na manispaa nyingine za jiji ambapo amewaonya watendaji wa manispaa kusimamia matumizi bora ya mkopo huo kwa ajili ya miradi iliyokusudiwa.
Bi. Mjema amewaonya watendaji wa manispaa hiyo kuhakikisha wanatumia ipasavyo pesa hizo na kwamba kamwe hatosita kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa wale watakaofuja au kutumia vibaya mkopo huo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, kupatikana kwa mkopo huo ni mafanikio makubwa katika kuhakikisha mandhari ya wilaya ya Temeke inafanana na ile ya wilaya nyingine kama Ilala na Kinondoni, kwani hivi sasa wilaya ya Temeke ipo nyuma kimaendeleo na imekuwa maarufu kwa takataka na mitaa isiyo na hadhi ya kuwa katika jiji ambalo ndio kitovu kikuu cha biashara nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa CRDB Dkt Charles Kimei amesema benki hiyo ni moja kati ya taasisi mbili za kifedha zilizopewa jukumu la kutoa huduma za kifedha kwa serikali za mitaa nchini na kwamba wakati wote wapo tayari kuhakikisha manispaa zinapata mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mkurugenzi huyo wa CRDB amesema mikopo kwa serikali za mitaa imekuwa ikisaidia sio tu maendeleo ya manispaa husika, bali hata ustawi wa sekta binafsi kwani miradi mingi ya maendeleo katika manispaa imekuwa ikitekelezwa na sekta binafsi.