Ijumaa , 2nd Feb , 2024

Serikali imetangaza kuacha kutumia nishati ya kuni kupikia chakula katika Magereza mbalimbali nchini ikiwa ni Utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango la Utunzaji wa Mazingira kwa kuacha kukata miti ili kutunza mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, akipanda mti katika Jengo jipya la Makao Makuu ya Wizara, Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma, leo Februari 2, 2024. Wanne kulia ni Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi hamad Masauni.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati akiongoza watumishi zaidi ya mia moja kupanda miti katika eneo la Ofisi ya Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma, Februari 2, 2024, ambapo  zoezi hilo pia lilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Jumanne Sagini, Katibu Mkuu, Kaspar Mmuya na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Abdallah Hassan Mitawi, ambapo zoezi la upandaji miti hiyo linafanyika kuelekea kuenzi Miaka 60 ya Muungano.

‘Nalipongeza Jeshi la Magereza na kuanza utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Dkt. Mpango ambapo aliagiza kuepuka matumizi ya kuni kwa sababu yanapelekea ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira ambapo dunia hivi sasa inakumbwa na janga la ukame huku sababu kubwa ikitajwa ukataji wa miti kwa matumizi mbalimbali’ alisema Waziri Masauni.

Akizungumzia zoezi la upandaji wa miti, Masauni amewataka watumishi kuhakikisha miti iliyopandwa na zaidi ya watumishi mia moja wa Wizara hiyo, inalindwa ili iweze kukua na kutimiza lengo la utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kaspar Mmuya amesema zoezi hilo litaendelea kwenye vyombo vilivyopo chini ya Wizara, ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

‘Sisi Wizara na vyombo vyote tunaenda kupanda miti katika maeneo husika huku Jeshi la Magereza wakiwa wameshapanda miti 800 na kufikia hadi kesho watakuwa wamepanda miti 1200 lakini vyombo vingine ndani ya mwezi huu wa pili watakua nao wamekamilisha upandaji wa miti kwa idadi ya miti watakayopangiwa ili tuweze kutekeleza agizo la Makamu wa Rais, Dkt. Mpango kupanda miti kuelekea sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ alisema Mmuya.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Abdallah Hassan Mitawi aliipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutekeleza agizo hilo huku akiwaasa watumishi kuhakikisha miti hiyo inakua ili iweze kuwa Faraja na urithi kwa vizazi vijavyo.