
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni amesema takwimu za ajali za barabarani hapa nchini kwa kipindi cha miaka mitatu zinatisha na jitihada za makusudi zinahitajika kunusuru hali hiyo.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoani Geita, Masauni ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema maisha ya watumiaji wa barabara yapo hatarini kutokana na makosa ya kibinadamu ambayo yamekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani.
“Matukio ya ajali kitakwimu kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2013 hadi Desemba 2015 yanatisha ambapo jumla ya ajali 46,536 zimesababisha vifo vya watu 11,230 na majeruhi 44,602"
Kwa kipindi hicho cha miaka mitatu vifo vya watembea kwa miguu ni 3,328, na majeruhi 8,256. vifo kwa wapanda pikipiki vilikuwa 2,493, na majeruhi 10, 702.
Kwa wapanda baiskel, vifo vilikuwa 1,071, majeruhi 2,060, huku kwa madereva wa magari ni vifo vikiwa 813 na majeruhi 3,157 na vifo kwa wasukuma mikokoteni vilikuwa 81 na majeruhi 246.
Aidha Waziri Masauni ametoa wito kwa wananchi wote kuchukua tahadhari wakati wa matumizi ya barabara na siyo kuwa na dhana kwamba jambo hilo ni kazi ya serikali pekee.
Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyuga ameishukuru serikali kwa kuufanya mkoa wa Geita kuwa eneo la kitaifa katika maadhimisho ya mwaka huu jambo ambalo litafanya wananchi waweze kujifunza zaidi sheria za usalama barabarani.