Alhamisi , 1st Dec , 2016

Waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba amesema maadili ya taifa lolote hayajengwi kwa sheria kali bali yanajengwa kwa jamii kusimamamia maadili huku viongozi wakitumia sheria hizo kutoa miongozo mbalimabli katika jamii husika.

Jaji Joseph Warioba

Amesema endapo hayo hayatazingatiwa ni dhahiri kuwa vita dhidi ya rushwa haitafanikiwa .

Mhe. Warioba amesema hayo katika kongamano lililoandaliwa na taasisi saba za serikali ikiwemo taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya maadili nchini.

Kwa upande wake Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora, Mhe. Angela Kairuki kupitia hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bi. Susan Mlawi amesema licha ya kuwepo na sheria na taratibu nyingi lakini tatizo la rushwa limeendelea kuwepo na hivyo jamii na taasisi husika ziongeze nguvu.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali CAG Prof.Juma Asad amesema vita ya maadili ni jambo muhimu katika jamii na hivyo ni jukumu la kila mtu kutambua kuwa uadilifu ni jambo la msingi zaidi na serikali pekee haiwezi kufanikisha.