Picha ya daladala zikiwa katika kituo cha mabasi zikisubiri abiria.
Baraza la Ushauri la watumiaji wa Huduma za Usafiri wa nchi Kavu na Majini (SUMATRA CCC) limeitaka Mamlaka ya usafiri wa nchi Kavu na majini (SUMATRA ) kwa kushirikiana na jeshi la polisi mkoani Mbeya kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kushinikiza wamiliki daladala kumaliza mgomo ulianza jumatatu wiki hii.
Mgomo huo ni ule ulioanza Jumatatu wiki hii na kusababisha adha kubwa ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Mbeya na vitongoji vyake.
Akiongea jijini Dar es salaam, Katibu Mtendaji wa SUMATRA CCC, Bw.Oscar Kikoyo amesema mgomo huo umewaathiri wakazi wa mkoani mbeya kwa kiwango kikubwa hali inayopelekea kuzorota kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
Kikoyo amesema mgomo huo ni batili kutokana na kukiuka sheria ya SUMATRA, sheria ya ushindani na kanuni za kutatua migogoro za mamlaka hiyo na nyinginezo za nchi.