Jumatatu , 16th Feb , 2015

Waziri wa Uchukuzi Mh Samuel Sitta amemsimamisha kazi kwa muda usiojulikana kaimu mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya bandari madeni kipande ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazomkabili ikiwemo ukiukwaji wa taratibu za manunuzi.

Waziri wa Uchukuzi Mh Samuel Sitta

Tuhuma nyingine zinazomkabili ni mahusiano yasiyoridhisha kati ya uongozi wa mamlaka hiyo na wadau wake muhimu ambapo pia mara kadhaa imetokea bodi inapopitisha wazabuni yeye huchelewesha barua, huku tume ya watu sita ikiundwa kuchunguza tuhuma hizo na Bw Awadhi Massawe akiteuliwa kushika wadhifa huo.

Wakati huohuo kamati ya bunge ya Hesabu za Serikali PAC imeitaka serikali kujenga bomba la kusafirisha mafuta kwenda mikoani ili kuepusha uharibifu wa barabara unaofanywa na malori yanayosafirisha mafuta ikiwa ni pamoja na kuwa na matenki makubwa ya umma ya kuhifadhia mafuta ili kupunguza msongamano wa meli za mafuta baharini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mh Zitto Kabwe ametoa wito huo mara baada ya kutembelea na kukagua eneo linalotumika kupokelea mafuta ambapo pia wameishauri serikali kufikiria chanzo maalum cha mapato kwa ajili ya ujenzi wa reli akitolea mfano nchi ya Kenya ambayo hutumia mapato ya kodi za bidhaa zinazotoka nje kupanua reli yao.

Akijibu maswali mbalimbali ya wajumbe wa kamati hiyo kaimu mkurugenzi wa TPA Bw Awadhi Massawe amesema asilimia 90 ya mizigo yote inayotoka bandarini inasafirishwa kwa njia ya barabara hivyo ni vyema serikali ikaweka mkazo kwenye ujenzi wa mabomba hayo pamoja na uimarishwaji wa miundombinu ya reli huku mwakilishi kutoka TRA akielezea utaratibu unaotumika kukusanya kodi.