Alhamisi , 23rd Mei , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mnghwira, ameeleza kuwa amepokea kwa masikitiko ajali ya moto iliyotokea leo Mei 23, 2019, kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Ashira iliyopo Marangu mkoani Kilimanjaro.

Ajali ya moto shule ya Ashira Marangu Moshi

Akiongea na www.eatv.tv muda mfupi baada ya moto huo uliounguza mabweni, Mh Mnghwira amesema bado hajapata tathmini kamili ya ajali, lakini Kamanda wa Polisi mkoani humo ambaye amewahi eneo la tukio, amemweleza kuna uwezekano mkubwa kuwa hakukuwa na mwanafunzi bwenini.

 
''Shule ya Ashira ni miongoni mwa shule kongwe ambazo zipo kwenye mpango wa kufanyiwa marekebisho na niliitembelea hivi karibuni, lakini nasikitika leo imeungua upande wa mabweni. Baadaye tutapata tathmini maana Kamanda yupo kule na RAS naye amekwenda'', ameeleza.

Mapema leo Mei 23, 2019, majira ya saa 6:00 mchana ulizuka moto shuleni hapo na kuunguza mabweni ya wanafunzi.