Jumamosi , 18th Oct , 2014

Walimu katika shule ya Msingi Pwani iliyopo Kata ya Kunduchi katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wanalazimika kutoroka vituo vyao vya kazi na kwenda mbali na mazingira ya shule kwa ajili ya kupata huduma za vyoo na maliwato.

Hali hiyo inatokana na uhaba mkubwa wa choo unaoikabili shule hiyo, ambapo zaidi ya wanafunzi mia nane pamoja na walimu Thelathini na Tatu wa shule hiyo, hutumia matundu yasiyozidi kumi ya choo, hali inayowaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko.

East Africa Radio imetembelea shuleni hapo na kushuhudia tatizo hilo kwani hata vyoo vilivyopo sasa vimechakaa na vinaweza kubomoka muda wowote kiasi cha kuhatarisha maisha ya wanafunzi wanaokwenda kujisaidia.

Aidha, choo kimoja ambacho kimetengwa kwa ajili ya walimu nacho hakitoshi kwani hutumiwa pia na walimu wa shule ya sekondari Pwani ambayo ipo jirani na shule hiyo.

Kutokana na uhaba huo, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi CCM kata ya Kunduchi, Bi Suzan Bakari amehamasisha wazazi kuchangia gharama za ujenzi wa vyoo vipya ambapo katika harambee iliyofanyika shuleni hapo leo, jumla ya fedha za Tanzania shilingi milioni Kumi zimepatikana kama ahadi na pesa taslimu kwa ajili ya ujenzi wa vyoo.

Kwa upande wao, vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM Kata ya Kunduchi wao wamejitolea matofali mia moja pamoja na jukumu la kuchimba mashimo yatakayotumika kwa ajili ya ujenzi wa vyoo hivyo.