Jumatano , 24th Nov , 2021

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko amesema katika wiki ya maadhamisho ya UKIMWI ambapo kitaifa mwaka huu inafanyika jijini Mbeya, zitafanyika shughuli mbalimbali ikiwemo Waziri Mkuu kuhudhuria Kongamano la Kisayansi juu ya mapambano ya VVU.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko

Dk. Leonard Maboko amesema hayo leo Novemba 24, 2021 kwenye uzinduzi wa wiki hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Tulia Ackson.

''Novemba 26 tutakuwa na kongamano la kisayansi katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kuweka mikakati. Hilo kongamano litazinduliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na litamalizika Novemba 27,'' ameeleza Mkurugenzi Mkuu wa TACAIDS Dk. Maboko.

Aidha, Dk. Maboko ameongeza kuwa, ''Kuna matukio mengi makubwa yatakuwa yanaendelea, wadau wote wanaoshughulika na mapambano dhidi ya UKIMWI wapo hapa kwenye mabanda. Pia kutakuwa na huduma mbalimbali ikiwemo kupima virusi vya UKIMWI, chanjo ya Uviko-19, shingo ya kizazi kwa kina mama, tohara kwa wanaume na mengine''.

Pia amesema kuwa, ''Asilimia karibu 40 ya maambukizi mapya yanatokea kwa vijana, hivyo Novemba 28, kutakuwa na Youth Dialogue, kwa vijana waliopo vyuo vikuu kujadiliana yale yanayoendelea kuhusu mapambano dhidi ya UKIMWI na ndio maana hapa kuna mabanda yanaitwa kijiji cha vijana''.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI, Jenard Lazaro ameeleza kuwa mfuko huo umekuwa msaada mkubwa katika kutokomeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

''Tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI mwaka 2015, kumekuwa na mafanikio mengi ikiwemo mfuko umeweza kutoa shilingi bilioni 1.1 kununua na kusambaza dawa za  magonjwa nyemelezi kwa watu wanaoishi na VVU, '' ameeleza  Lazaro.