Hospitali hiyo iko katika mji wa Mrauk-U katika jimbo la Rakhine, eneo linalodhibitiwa na Kundi la Arakan - mojawapo ya makundi yenye nguvu zaidi ya kikabila yanayopigana na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
Maelfu wamefariki dunia na mamilioni wamekimbia makazi yao tangu jeshi lilipochukua nchi katika mapinduzi ya mwaka 2021 na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi limeongeza mashambulizi ya anga ili kurudisha maeneo kutoka kwa makundi ya kikabila.
Jeshi la Myanmar halijatoa kauli yoyote kuhusu mashambulizi hayo, ambayo yanakuja huku nchi hiyo ikijiandaa kupiga kura baadaye mwezi huu katika uchaguzi wake wa kwanza tangu mapinduzi.
Hata hivyo, akaunti zinazounga mkono jeshi kwenye Telegram zinadai shambulio hilo halikuwalenga raia.
Wanajeshi wako katika mzozo wa miaka mingi wa umwagaji damu dhidi ya wanamgambo wa kikabila, wakati mmoja jeshi lilipoteza udhibiti wa zaidi ya nusu ya nchi.
Ikumbukwe Serikali ya Myanmar imeitisha uchaguzi mkuu tarehe 28 Disemba, na kuutaja kama njia ya kuleta utulivu wa kisiasa. Lakini wakosoaji wanasema uchaguzi hautakuwa huru wala wa haki.
Makundi ya kikabila na makundi mengine ya upinzani yameahidi kususia uchaguzi huo.




