Jumatano , 26th Oct , 2016

Shirika la Plan International limetoa rai kwa serikali kuanzisha idara ya kazi katika maeneo ya migodi ili ishirikiane na wachimbaji wa madini kuhakikisha tatizo la ajira kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 linakoma.

Kazi ya uchimbaji ikiendelea mgodini

Rai hiyo imetolewa leo mkoani Geita na Mratibu wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto wa shirika hilo, Maxmillian Kitigwa alipokuwa akiongea na wanahabari kuhusu changamoto zinazoukabili mradi huo.

Bw. Kitigwa amesema, katika Mkoa huo kuna changamoto nyingi zinazowakabili watoto lakini kukosekana kwa Idara ya Kazi katika maeneo ya migodi kunasababisha uvunjwaji mkubwa wa haki za watoto kwa kuwa watoto wengi wanakimbilia kufanya shughuli mbalimbali katika maeneo hayo ili kujipatia kipato.

Amesisitiza kwamba, sasa hivi Geita ni mkoa ambao u umezungukwa na migodi mikubwa hivyo Serikali haina budi kuweka Idara ya Kazi katika maeneo hayo ili kuzuia ajira za watoto pamoja na kukomesha unyanyaswaji unaofanywa kwa baadhi ya watu wanaofanya kazi huko