Jumatatu , 10th Nov , 2014

Wananchi kutoka maeneo mbali mbali ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam, leo wamekusanyika nje ya kituo cha tiba mbadala cha Fore Plan Clinic inachomilikiwa na Dkt Juma Mwaka Juma, wakiitaka serikali ikifungulie kituo hicho.

Alhamisi ya juma lililopita, wizara ya afya na ustawi wa jamii ilitangaza kuifunga kwa muda kliniki ya Fore Plan kwa madai ya kutokidhi viwango vya utoaji huduma ya tiba na afya.

Wananchi kutoka maeneo mbali mbali ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam, leo wamekusanyika nje ya kituo cha tiba mbadala cha Fore Plan Clinic inachomilikiwa na Dkt Juma Mwaka Juma, wakiitaka serikali ikifungulie kituo hicho baada ya wizara ya afya na utawi wa jamii kukifunga wiki iliyopita.

Wananchi hao ambao wengi wao wakiwa ni akina mama wamesema kufungwa kwa kituo hicho ni pigo kwao kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiitegemea kliniki hiyo kama kimbilio lao kwa tiba za matatizo ya uzazi, hasa kutokana na ukweli kwamba baadhi yao ndoa zao zipo hatarini kuvunjika kutokana na kukosa watoto.

Kwa mujibu wa akina mama hao, kufungwa kwa kituo hicho ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwani hakujazingatia kuwa kuna watu walikuwa wanaendelea na matibabu na kwamba kuna haja ya kukifungulia haraka iwezekanavyo.

Wakizungumza kwa uchungu mkubwa nje ya ofisi za kliniki hiyo zilizopo Ilala Bungoni jijini Dar es Salaam, akina mama hao wamesema badala ya kuifungia kliniki hiyo, ni bora serikali ingeenda kuzifungia nyumba za kulala wageni maarufu kama gesti bubu, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa chanzo cha maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.

Akizungumzia sakata hilo, Dkt Mwaka mwenyewe amelalamika kuathirika kibiashara, kwani kwa muda wote ambao kituo hicho kimefungwa, amejikuta akilazimika kulipia huduma na gharama nyingine ikiwemo mishahara kwa watumishi zaidi ya arobaini wa kituo hicho, hali aliyodai kuwa imemsababishia hasara ya kiasi kikubwa cha pesa.