Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
Dkt. Biteko amesema hayo leo (Mei 11, 2024) Jijini Dodoma alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgemi rasmi katika maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania ambapo amesema huduma zinazotolewa na chama hicho zinazingatia sheria na kanuni na taratibu za kuanzishwa kwa chama hicho ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bila upendeleo.
‘‘Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kukiwezesha chama hiki kwa namna mbalimbali,…ombi lenu la Serikali kuwapatia ruzuku katika shughuli muhimu za jamii yetu tumelipokea na tunalifanyia kazi. Hadi sasa kuna ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa Chama cha Msalaba Mwekundu na viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali. Kila tunapofanya ziara tunashirikiana na nawaona kwenye shughuli za Serikali iwe sherehe, misiba ya kitaifa mkitoa huduma ya kwanza kwa washiriki, wakati wa majanga mbali mbali tunawashuhudia mkitoa huduma’’, amebainisha Dkt. Biteko.
Ametaja baadhi ya huduma zinatolewa katika nyakati mbalimbali ‘‘Chama hiki kimekuwa kikitoa huduma ya kwanza kwenye majanga mbalimbali yaliyotokea kama vile mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyotokea Hanang - Katesh, kuimarisha huduma za afya kwa kujenga wodi za wazazi na wodi za watoto na kina mama na kutoa vitendanishi, vifaa kinga na vifaa tiba, pamoja na kushiriki katika utoaji wa huduma za afya katika makambi ya wakimbizi’’, amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza ‘‘Serikali pia inatambua na kuthamini ushiriki wenu mkubwa mlioonesha kwenye maporomoko ya udongo yaliyotokea katika mlima wa Hanang – Katesh na juhudi zinazoendelea hivi sasa za kuisaidia Serikali kujenga nyumba 35 kati ya nyumba 101 za wahanga wa maporomoko hayo kama alivyoagiza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan’’.
Kufuatia jitihada za Chama cha Msalaba Mwekundu nchini ambacho ni kielelezo cha utu na ukarimu kwa binadamu, vile vile ni ishara ya uzalendo mkubwa, Desemba 12, 2023 Rais Dkt. Samia alitoa cheti cha kuwapongeza kwa kutambua mchango wao katika kushughulikia maafa ya mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewahimiza watanzania kuendelea kuiombea nchi kipindi hiki kuelekea Uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 waendelee kuiombea Tanzania ili uchaguzi huo ufanyike kwa Amani na usalama.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Red Cross Tanzania katika kuwasaidia wananchi wanaokumbwa na changamoto mbalimbali za majanga ambayo yamekua yakitokea kutokana na mabadiliko ya tabia nchi au kwa namna yeyote ile na kuwa viongozi wa umma wanapaswa kuwahudumia wananchi kwa furaha.
"Watanzania tumekuwa na moyo wa kujitoa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere Tanzania ilipopata uhuru ilijitoa kusaidia mataifa mengine, viongozi lazima kujitoa katika kufanya huduma na kazi zilizo mbele yetu kwa Watanzania milioni 61 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, tutoe uwezo wetu na nguvu zetu zote kuwasaidia", amesema Balozi Chana.
Naye, Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihanzile ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana nao na kuimarisha huduma mbalimbali nchini mfano kwa kujenga hospitali, shule na barabara.
"Mtoto akikosa tiba amepungukiwa huduma za kibinadamu, akikosa shuleni tunatakiwa tumsaidie, majanga kama maafa yanapoongezeka kwetu tunahusika, njaa au upungufu wa damu unapotokea ni jukumu letu kusaidia, ukimpata kiongozi ambaye mipango na maono yake inakwenda kupunguza haya, basi anawapunguzia kazi”, amesema Mhe. Kihanzile.
Amefafanua “Baada ya miaka zaidi ya 40 Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kinamkabidhi tuzo maalum kwa mtu mmoja tu, tuzo ya ubinadamu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni kutambua na kuheshimu mchango wake".
Mwakilishi wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Uganda, Bw. Halid Kirunda amesema kuwa nchi za Afrika Mashariki zimekua zikishirikiana katika shughuli za utoaji huduma za maokozi kwa kuzingatia sheria za haki za binadamu zinavyoelekeza kwakua ni kiunganishi baina ya wananchi na Serikali.
Sambamba na mafanikio mbalimbali aliyoyataja ambayo yamechangiwa na Chama hicho ameziomba Serikali kuendelea uwezeshaji wa fedha na vifaa vya shughuli za uokozi kwa kuwa baadhi ya vyama hivyo vinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha za kutosha na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uokozi.
Ameongeza kuwa msingi wa Chama cha Msalaba Mwekundu ni kutoa huduma za uokozi bure bila kubagua maeneo yakufika kwa vile wanatanguliza utu mbele na kazi hiyo wanaifanya kwa kujitolea hivyo ni vyema kuwasaidia watoa huduma hao kumaliza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ambazo zinawapa ugumu wakutekeleza majukumu yao.