Jumatano , 15th Oct , 2014

Serikali ya Tanzania kupitia ofisi ya waziri mkuu imeandaa mfumo wa uboreshaji wa taarifa za tabia nchi na kuboresha mifumo ya tahadhari ili kuwanusuru wananchi dhidi ya majanga yanayowagharimu kiuchumi kama vile mafuriko na ukame.

Mpango huo wa miaka minne, utawasaidia wakulima kupata taarifa za hali ya hewa ili waweze kuzitumia kupanga kilimo chenye tija pamoja na kuepuka hasara za mafuriko na ukame.

Mratibu wa mradi huo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Alfei Daniel amesema wafugaji nao kwa upande wao watanufaika na taarifa hizo ambazo zitawasaidia kuinua pato lao, la familia zao na la taifa kwa ujumla.

Tanzania ni moja ya nchi zinazotekeleza miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi yakiwemo majanga kama milipuko ya magonjwa, ukame uliokithiri pamoja na mafuriko.