Rais Magufuli akiwa na maafisa na viongozi wengine mbalimbali akikata utepe kuzindua rasmi ndege mbili mpya za serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam Septemba 28, 2016
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Rais Magufuli amelitaka shirika hilo kuweka nidhamu ya utendaji kazi kupitia ndege hizo ili kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa kisasa nchini.
Rais Magufuli amesema kuwa mbali na ndege hizo mbili ambazo zitakuwa zinafanya safari zake nchini Tanzania, serikali ina mpango wa kununua ndege nyingine mbili zenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 150 na kuendelea ili kuboresha zaidi usafari wa anga kuwa na kuleta ushindani wa kibiashara kimataifa.
Amesema katika ndege hizo, moja itakuwa na uwezo wa kubeba watu 160 na nyingine watu 240 zikiwa na uwezo wa kutoka Marekani, China na Uingereza moja kwa moja hadi Tanzania na kwamba pesa zipo, na kinachofanyika hivi sasa ni mazungumzo ili utengenezaji wa ndege hizo usichukue muda mrefu.
Rais Magufuli amefafanunua juu ya kununua ndege hizo kwa fedha taslim badala ya mkopo kuwa ni kutokana na gharama nafuu waliyoipata katika ununuzi wa ndege hizo, ambapo amesema kununua kwa fedha taslim ni nafuu zaidi kuliko kununua kwa mkopo.
Rais Magufuli amewataka Watanzania kushikamana kwa pamoja kwa maendeleo ya taifa na kuacha kubeza kila jambo la maendeleo linalofanywa na serikali hatua ambayo inadhoofisha jitihada za serikali katika kuleta maendeleo.
Eatv ilifanya mahojiano baada ya uzinduzi huo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Magembe amesema ujio wa ndege hizo utachochea safari za watalii katika mbuga za wanyama ambazo zilikuwa azifikiwi kirahisi akitolewa mfano Kisiwa cha Mafia na zitapunguza gharama kubwa ya safari za ndani za watalii.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo nao wametoa maoni yao juu ya ndege hizo, ambapo Bw. Saidi Kiame Mkazi wa Temeke amemtaka Rais Magufuli kuendelea na kasi hiyo ili kuwaletea wananchi maendeleo huku Bw. Selemani Mabegeli akipongeza hatua hiyo.