Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na mwekezaji mzawa kwa kushirikiana na Wachina, inatarajiwa kukamilika Oktoba, mwaka huu ambapo fedha hizo zitapatikana baada ya kukamilika awamu tatu za ujenzi wake.
Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetembelea kiwanda hicho jana, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Bw. Mohammed Kiluwa alisema ujenzi huo utasaidia kuimarisha uchumi.
“Kukamilika kwa mradi huo, kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi, upatikanaji wa ajira pamoja na kufanikisha azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya maendeleo ya viwanda,” alisema.
Alisema kiwanda hicho kitazalisha nondo kwa matumizi ya ujenzi pamoja na vifaa vingine vinavyohusiana na bidhaa za chuma. “Lengo ni kuweza kuuza malighafi hizo kwenye viwanda vingine vya chuma nchini na nchi jirani kwa kuzingatia ubora unaokidhi mahitaji ya soko la kimataifa,” alisisitiza.
“Katika awamu ya kwanza ya ujenzi, tunatarajia kutumia dola milioni 40; awamu ya pili tutatumia dola milioni 50 na dola milioni 200 zitatumika kwenye awamu ya tatu ili kukamilishia ujenzi wa kiwanda hiki,” alisema.
Kiluwa alisema, awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu, ambapo awamu ya tatu itakamilika Februari mwakani. Kikikamilika, kinatarajiwa kuajiri vijana zaidi ya 500 wa Kitanzania.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kikubwa cha kwanza kinachojengwa na mwekezaji mzawa.
“Uwekezaji sio lazima ufanywe na watu wa nje, Watanzania wana nafasi ya kuwekeza katika sekta mbalimbali, Kiluwa amefungua njia hivyo wengine wafuate nyayo zake. Uwezo tunao na sababu ya kuwekeza tunayo, kwani tunataka tuzalishe bidhaa mbalimbali sisi wenyewe,” alisema.
Aliongeza kuwa uwepo wa kiwanda hicho katika eneo la Disunyara, Mlandizi mkoani Pwani, utawezesha kuboresha hali ya uchumi kwa wakazi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.
Waziri Mkuu alitolea mfano kwa wakazi wa Mtwara, ambao wamenufaika kutokana na ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote ambapo awali walikuwa wakinunua saruji kwa sh. 17,000, lakini hivi sasa wanainunua kwa sh. 7,000.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lipeleke umeme mapema kwenye eneo hilo ili kuharakisha shughuli za uwekezaji.