Jumapili , 12th Sep , 2021

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema Serikali inaandaa utaratibu wa wiki ya uchanjaji ambayo inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Septemba au mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa

Msigwa ameyasema hayo leo Jumapili Septemba 12, 2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya wiki.

''Serikali moja ya vitu ambayo inaviangalia kwasasa ni kuhakikisha tunakuwa na wiki ya uchanjaji. Utaratibu huu sasa unaandaliwa bila shaka mwishoni mwa mwezi wa 9 au mwanzoni mwa mwezi wa 10, tutakuwa na wiki ya uchanjaji, ambapo viongozi wa nchi nzima watashiriki kwenye wiki hivyo kuhakikisha watanzania wengi wanapata chanjo,'' amesema Gerson Msigwa, Msemaji Mkuu wa Serikali.

Aidha ameeleza kuwa ''Wataalam wetu wanatuambia watu ambao hawajachanjwa wakiugua Uviko-19 wanapata madhara makubwa na wengine wanapoteza maisha lakini waliochanjwa wanatibiwa na wanarudi nyumbani''.

Kuhusu mwenendo wa chanjo, Msigwa amesema, ''Tumefika asilimia kama 34 ya zile chanjo Milioni 1,054,400 zilizoletwa. Watanzania takribani laki 345,000 wameshapata chango hiyo, lakini pia Serikali inaendelea kuangali namna ya kuleta chanjo zingine ili watanzania waweze kupata chanjo''.