Jumapili , 5th Oct , 2014

Serikali nchini Tanzania imesema mchakato wa kuandaa sheria itakayohusu usimamizi wa masuala ya ardhi itakayolenga kuondoa migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza kwa sasa ikiwemo ya wananchi na wawekezaji pamoja na wakulima na wafugaji.

Akizungumza mjini Morogoro Mwanasheria wa wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Charles Mpaka amesema kukamilika kwa sheria hiyo kutafanya uzalishaji wa chakula na uwekezaji kufanyika bila migogoro ili kuleta manufaa kwa taifa zima

Bw. Mpaka ameongeza kuwa sheria hiyo itawezesha Ardhi ya kilimo kulindwa, Kuainishwa pamoja na kupimwa na kutengewa madaraja maalumu kwa ajili ya kuwezesha watu watakaotumia ardhi hiyo kufuata kanuni bora ndani ya nchi yetu.

Wakati huo huo, Mamlaka ya maji ya mji mdogo wa USA RIVER Wilayani Arumeru Jijini Arusha nchini Tanzania imelalamikiwa kwa kushirikiana na baadhi ya watu kuhujumu miundo mbinu ya maji ili waweze kujipatia fedha wakati wanapohitaji kutengeneza miundombinu hiyo.

Akijibu shutuma hizo Meneja wa mamlaka hiyo Bw. Daniel Ndeku amekiri kupokea malalamiko hayo na tayari ameshaanza kuyafanyia kazi na kusema kuwa lipo tatizo la wakandarasi wanaopewa kazi ya ujenzi wa barabara kutojali miundombinu ya maji.

Kwa upande wake mtaalamu wa ufundi Sekta ya Barabara Bw. Robert Gadi amesema tatizo la ukataji wa mabomba ya maji wakati wa utengenezaji barabara linatoka na utaratibu wa baadhi ya wananchi kutofuata taratibu wakati wa kuunganishiwa huduma hiyo.