Mbunge Tundu Lissu alipokuwa akipata matibabu Hospitali ya Nairobi
Dk. Possi ametoa tamko hilo wakati akijibu madai ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyoyatoa hivi karibuni nchini humo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha News Africa cha kituo cha televisheni cha Deutsche Welle (DW).
Akijibu madai ya Lissu katika tamko lake la Januari 29, 2019, Dk Possi amesema Serikali imekuwa ikilifuatilia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuanza uchunguzi na kwamba amesema mamlaka za Serikali zingetaka kumpata Lissu ili atoe ushirikiano.
“Hadi sasa vyombo vya sheria havijapata ushirikiano wa mbunge huyo na dereva wake ili kupata taarifa muhimu za siku hiyo. Uchunguzi kwa Tanzania bado ni muhimu na bado unawasubiri wao kwa kuwa walishuhudia kwa macho ili waeleze kilichotokea,” ameongeza Dk Possi.
Aidha Balozi Possi amemtaka Mbunge huyo kupima ishara njema za Rais na kwamba kwenye madai anayotoa hayana msingi.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa taarifa ya kulaani tukio hilo na kuagiza uchunguzi wa kina wa haraka. Kwa nyakati tofauti Rais amemtuma Makamu wake, Rais mstaafu na viongozi wengine wa Serikali kumtembelea Lissu akiwa hospitali akiwa Dodoma, Nairobi na Brussels (Ubelgiji).” Dk. Possi

Dkt. Possi.
Naye Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbas katika ukurasa wake wa Twitter ameeleza kwamba "bado ubalozi unasubiri miadi ya DW kutoa tarehe kwa mahojiano kufafanua zaidi".
UPDATE
Baada ya Kauli za Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dkt. Abdallah Possi kufunguka kuhusu kushindikana kufanyika uchunguzi kutokana na kukosa ushirikiano kwa Mbunge Lissu, kiongozi huyo na mwanasheria, amesema kwamba Sheria ya kusaidiana katika masuala ya jinai iliyotungwa na Bunge la Tanzania, imeweka utaratibu wa namna ya kupata ushahidi au mtuhumiwa aliyeko nje ya Tanzania.
Ameeleza kwamba "Mwanasheria Mkuu wa Tanzania anatakiwa kuomba msaada wa nchi aliko shahidi au mtuhumiwa huyo ili kupatikana ushahidi au mtuhumiwa anayehitajika kwa uchunguzi wa kijinai. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania hajawahi kuomba msaada wa Serikali ya Kenya, kwa kipindi chotenilichokuwa nimelazwa Nairobi".
Aidha Lissu ameongeza kwamba “Jeshi la Polisi halijawahi kueleza hata aina ya silaha au risasi zilizotumika kunishambulia, taarifa ambazo hazihitaji uwapo wangu, bali uchunguzi wa kitaalamu wa silaha, lakini pia halijawahi kueleza nani aliyeondoa CCTV iliyokuwapo kwenye jengo la makazi yangu baada ya shambulio kwa nini iliondolewa mahali ilikopelekwa, na ni kitu gani kinaonyeshwa kwenye CCTV hiyo,” amesema Lissu
“Kwa hiyo, katika mazingira haya, kauli ya Balozi Possi kwamba uchunguzi wa shambulio dhidi yangu unasubiri mimi na dereva wangu turudi Tanzania, ni kauli ya kukwepa kuwajibika kwa vyombo vya upelelezi vya Serikali ya Tanzania" Amesisitiza Mbunge huyo ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA.
Lissu kwa sasa yuko nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu kufuatia shambulio la risasi la Septemba 7, 2017 jijini Dodoma.





