Jumanne , 12th Jan , 2016

Chama cha Wananchi (CUF) kimemuomba Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia moja kwa moja mazungumzo ya kusaka suluhisho la mkwamo wa kisheria na kikatiba visiwani Zanzibar.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa CUF ambaye ndiye aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ametupilia mbali uwezekano wa kurejewa uchaguzi kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Maalim Seif amesema kuna kila dalili kuwa Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye anaongoza mazungumzo visiwani Zanzibar hataki kuitisha kikao cha mwisho kupokea tathmini ya vikao nane vilivyokwishafanyika tangu vilipoanza mwanzoni mwa mwezi Februari na badala yake wasaidizi wake wanaandaa uchaguzi wa marudio kinyume cha sheria, jambo ambalo CUF haiko tayari.

Maalim Seif amesema kuwa hoja ya kurudia uchaguzi sio suluhisho la kutatua mgogoro huo na kuainisha kuwa ana imani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta John Pombe Magufuli katika kupata ufumbuzi wa mgogoro huo kuwa ana nia njema.