Ijumaa , 1st Apr , 2022

Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania na Mwanachama wa muda mrefu wa Chama cha Mapinduzi Mzee Yusuph Makamba amesema tangu Rais Samia Suluhu Hassan achaguliwe na Mungu kuwa Rais wa Tanzania, sasa Watanzania wanalamba asali.

Mzee Yusuph Makamba, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM

Mzee Yusuph Makamba ameyasema hayo leo April 1, 2022 Jijini Dodoma wakati alipopewa nafasi ya kumsemea Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kanali Abdulrahman Omari Kinana kabla ya kufanyika kwa zoezi la kupiga kura katika mkutano Mkuu wa CCM unaofanyika Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma. 

Mzee Makamba amesema kwamba, alimtumia Rais Samia ujumbe na kumwambia kuwa anamshukuru Mungu kwa kumchagua Rais, ameendelea kusema kwamba alimtumia pia ujumbe mdogo wake Rais wa Zanzibar, Rais Mwinyi na kumshukuru Mungu kwa kumchagua Rais.

"Ulipochaguliwa kuwa Rais nilikuletea meseji na hata mdogo wangu Mwinyi nilikuletea meseji. Nikasema hivi, asante Mungu kwa kutuchagulia Rais" - Mzee Makamba

Hata hivyo, Mzee Makamba amesema kuwa baada ya kuchaguliwa kwa Rais Samia sasa Watanzania wanalamba asali na kuuhoji mkutano huo kama wanalamba asali. 
"Kwahiyo sasa hivi tunalamba asali watoto wanasoma tunalamba asali, tunapata maji tunalamba asali, umeme tunapata, tunalamba asali, niliposema tutalamba asali sikukosea. Wenzangu hamlambii? Hamlambi asalii?" - Mzee Makamba.

Aidha, baada ya uchaguzi huo uliofanywa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM, Abdulrahman Omari Kinana ameshinda kwa asilimia mia moja kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa akishika mikoba ya Mzee Philip Mangula ambaye ameng'atuka.