Jumatatu , 19th Aug , 2024

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Camillus Wambura amemhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACP Theopista Mallya kwenda Makao Makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP George Katabazi. 

Jeshi la Polisi Tanzania limeomba radhi kutokana na kauli aliyoitoa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Theopista Mallya ambapo amenukuliwa na vyombo vya habari kadhaa akisema kuwa binti aliyebakwa "alikuwa kama anajiuza". Polisi wamesema kuwa kauli hiyo sio msimamo wa Jeshi hilo

Kauli hiyo imefuatia baada ya RPC kuzungumza na chombo cha Habari hapa nchini kwa njia ya simu ambapo aliulizwa ikiwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na swali lingine aliloulizwa ni madai ya binti huyo kujiuza ambapo majibu ya kamanda huyo alisema hata kama ni hivyo hangestahili kutendewa hivyo. 

“Jeshi la Polisi lingependa kuomba radhi kwa kila mmoja aliyeguswa na kuchukizwa na kauli hiyo inayosambaa kwenye vyombo vya Habari wakati ufuatiliaji ukifanyika kupata usahihi wake,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi.