Ijumaa , 23rd Oct , 2020

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, amesema serikali ya mkoa huo imejipanga kukabiliana na vijana 150 walioandaliwa kila Kata na vyama vya upinzani kwa ajili ya kufanya vurugu kwenye vituo vya kupigia kura siku ya Oktoba 28,2020, wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 23, 2020, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, na kuelezea hali ya ulinzi na usalama kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo amesema wanazo taarifa za makundi hayo kupanga njama za kufanya maandamano, kufunga barabara na kuwafanyia vurugu wasimamizi wa Uchaguzi kwenye vituo.

"Inasemekana kwamba kuna baadhi ya vijana 150 ambao wameandaliwa katika kila Kata, ambao watakuwa wanazunguka na bodaboda kwenye vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kutishia wapiga kura na kuufanya mji uonekana hauna amani, niwaombe wananchi amkeni Alfajiri mkapige kura na mkimaliza mrudi nyumbani", amesema RC Chalamila

Aidha amewahamasisha wananchi kujitokeza kwenye vituo vya kupigia kura na kwamba mara baada ya kukamilisha zoezi hilo warudi nyumbani kuendelea na majukumu mengine na kutokubali kubaki vituo kwa madai ya kulinda kura kwani sio jukumu lao.