Aliyekuwa Rais wa Chad Idriss Deby
Deby alienda mstari wa mbele mwishoni mwa wiki kuvitembelea vikosi vya nchi hiyo ambavyo vinapambana na waasi kaskazini mwa nchi hiyo. Waasi hao wamevuka mpaka wakitokea nchi ya Libya.
Kifo chake kimetokea ikiwa ni saa chache tu tangu matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika Aprili 11 kuonesha kuwa anaongoza kwa asilimia 80. Kwa ushindi huo, Deby angeiongoza nchi hiyo kwa awamu ya sita mfululizo.
Serikali na bunge limevunjwa na sasa baraza la kijeshi ndilo litakaloiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miezi 18 ijayo.
Waasi hao wa kundi linalojiita Fact (the Front for Change and Concord in Chad), walishambulia kambi ya mpaka wa Libya na Chad siku ya uchaguzi, yaani Aprili 11. Walikuwa wakisonga mbele kuelekea mji mkuu wa N'Djamena.
Mapambano baina ya waasi na wanajeshi wa serikali yalianza siku ya Jumamosi. Jenerali wa jeshi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa waasi 300 waliuawa na wengine 150 kukamatwa katika mapambano hayo.
Aliongeza kuwa jeshi lilipoteza askari watano na wengine 36 wakijeruhiwa. Hata hivyo idadi hiyo haikuweza kuthibitishwa mara moja na chombo huru.