Jumatano , 25th Jun , 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana amewaapisha Wajumbe na Katibu wa Tume ya Kuchunguza Operesheni Tokomeza katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Aidha, Rais Kikwete amemwapisha Ofisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje, Joseph Edward Sokoine kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Wajumbe wa Tume ya Tokomeza walioapishwa ni Jaji Mstaafu Hamisi Amiri Msumi ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo na Majaji Wastaafu Stephen Ernest Ihema na Vincent Damian Lyimo ambao wanakuwa wajumbe wa Tume hiyo. Katibu wa tume hiyo ambaye pia ameapishwa na Rais Kikwete ni Bwana Frederick Kapela Manyanda.

Wajumbe pamoja na Katibu wa tume waliteuliwa karibuni na Rais Kikwete ili kufanya uchunguzi n akubaini ukweli wa jinsi Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa kufuatia malalamiko yaliyotokana na Operesheni hiyo ambayo ililenga kukabiliana na ujangili wa wanyamapori nchini.