Jumanne , 27th Jul , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali iliweka uwepo wa tozo za uzalendo kwenye miamala ya simu kwa lengo la kukusanya fedha zitakazosaidia katika ujenzi wa barabara vijijini pamoja na upatikanaji wa huduma za maji katika maeneo hayo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 27, 2021, Jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuwaapisha mabalozi 13 wa nchi mbalimbali aliowateua siku za nyuma na kuongeza kuwa Julai 29 mwaka huu atapokea maoni ya kamati aliyoiunda kuhusu miamala ya simu.

"Makato haya tuliyaweka kwa nia njema tu nchi yetu sasa hivi wakulima wameamka na kilimo kikubwa lakini wakivuna wanashindwa kuyaleta mavuno kwenye masoko tatizo ni njia kwa hiyo sehemu kubwa ya pesa hii itakwenda kwenye kujenga njia za vijijini, tumesikia vilio vya Watanzania, tozo zipo ila tutaangalia njia nzuri ambayo haitaumiza watu, serikali ipate na maendeleo yaendelee," amesema Rais Samia.