
Nyumba aliyokuwa amehifadhiwa Mfanyabiashara Mo Dewji alipotekwa, iliyopo Mtaa wa Mwansasu Mbezi Beach, jijini Dar es salaam.
Leo Jumapili Novemba 11, 2018 mbele ya wanahabari, Kamanda Mambosasa ameonyesha nyumba hiyo yenye ghorofa moja iliyopo Mtaa wa Mwansasu Mbezi Beach jinini humo.
Amesema baada ya mfanyabiashara huyo kupatikana polisi waliendeleza msako na kufanikiwa kuipata nyumba hiyo iliyopo umbali kilomita moja toka barabara ya Old Bagamoyo.
"Nyumba hii ndipo alipokuwa akihifadhiwa Mo baada ya kutekwa, Nyumba hii ni ya marehemu Mwansasu lakini sasa hivi inamilikiwa na binti zake, katika nyumba hii walitokea watu waliojitambulisha kuwa ni wafanyabiashara wa madini kutoka Afrika Kusini walipanga lakini walipitia kwa Twalib Mussa," amesema.
Kamanda Mambosasa amesema makubaliano yaliyokuwapo ni wafanyabiashara hao kulipa Dola za Marekani 1,500 (shilingi milioni 3.4) kwa mwezi huku wahusika wa nyumba wakipata dola 1,300 huku Mussa aliyefanikisha wafanyabiashara kupata nyumba hiyo akiambulia dola 200.
Kwa upande wake, Twalibu ambaye ni dereva wa teksi anayefanya shughuli zake Hotel ya Whitesands amesema yeye ndio aliyefanikisha wafanyabiashara hao kupata nyumba hiyo baada ya kuwaunganisha na madalali.
Mfanyabiashara Mo Dewji alitekwa Oktoba 11,2018 alfajiri katika hoteli ya Colosseum, alikokwenda kufanya mazoezi lakini alipatikana Oktoba 20 katika viwanja vya Gymkhana baada ya kutelekezwa na watekaji.