Jumatatu , 27th Oct , 2014

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limeendesha operesheni maalum ya kutokomeza bangi katika mkoa huo, kwa kuteketeza hekari Tano za mashamaba ya bangi mkoani humo.

Baadhi ya wananchi wa tarafa ya Mgeta wilayani Mvomero na maeneo mengine mkoani Morogoro, wameacha shughuli halali za uzalishaji mali na kuchangia maendeleo ya huduma muhimu kama za elimu na afya, badala yake kuelekeza nguvu zao kwenye kilimo haramu cha bangi katika mashamba yaliyopo milimani ambako sio rahisi kufikika.

Jeshi la Polisi limeendesha operesheni maalum ya kutokomeza bangi katika baadhi ya maeneo ikiwemo katika milima ya Kikewe na Mgeta, ambapo imeshuhudia bangi hiyo ikiwa imestawi mashambani, huku wahusika wa mashamba hayo wakikimbia kusikojulikana.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kikewe, Said Rashid, amesema kilimo hicho kimekuwa kikirudisha nyuma hata masuala muhimu kama ya elimu, kwa wananchi kuacha kulima mazao ya chakula na biashara na kushindwa kujitolea nguvu kazi kuchangia maendeleo yakiwemo ya elimu katika eneo hilo.

Wananchi waliohojiwa kuhusiana na kilimo hicho na nani wanaohusika na ulimaji huo wa bangi au kumiliki mashamba katika maeneo hayo ambayo kijiografia sio rahisi kufika kirahisi, wengi wameshindwa kutoa ushirikiano, huku mkazi mmoja yeye akikiri kilimo hicho cha bangi kimewaingiza vijana wengi kwenye uvutaji, jambo linalosababisha mifarakano na vurugu za mara kwa mara kwa baadhi ya familia, wakiwemo vijana kuwapiga wazazi wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Leonard Paulo, amesema jumla ya hekari Tano za mashamba ya bangi zimeteketezwa katika wilaya za Mvomero, Kilosa na halmashauri ya wilaya ya Morogoro ambapo watu wanne Tekla Andrea, Feldinand Mlovosa, Alex Gilbert na Erasto Sanga, wakazi wa chabima wilayani Kilosa wanaodaiwa kumiliki mashamba hayo wanashikiliwa na Polisi na watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa.